Ufaransa Waafrika ni wawili tu

Picha 
WAAFRIKA wengi wameungana na raia wa Ufaransa kushangilia ubingwa wa Kombe la Dunia walioupata timu ya taifa ya nchi hiyo Jumapili iliyopita. Ufaransa waliibuka mabingwa wapya baada ya kuwalaza Croatia mabao 4-2 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa mjini Moscow, Urusi.
Waafrika wengi wamekuwa na furaha baada ya Ufaransa kulichukua kombe hilo kutokana na timu hiyo kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wenye asili ya Afrika. Kati ya wachezaji 23 waliounda kikosi cha timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Dunia, wachezaji 13 wana asili ya Afrika.
Wachezaji hao ni Presnel Kimpembe, Samuel Umtiti, Paul Pogba, Thomas Lemar, Kylian Mbappe, Ousmane Dembéle, Corentin Tolisso, N’Golo Kante, Blaise Matuidi, Steven Nzonzi, Steve Mandanda, Djibril Sidibe na Benjamin Mendy. Licha ya wachezaji wote hao kuwa na asili ya Afrika lakini ni wawili tu ndio walioonja joto la bara hili nikimaanisha kuwa wamezaliwa huku, lakini waliobaki wote wamezaliwa Ufaransa na kukulia nchini humo.
Waliozaliwa Afrika ni beki kisiki, Samuel Umtiti ambaye alizaliwa Cameroon pamoja na mlinda mlango, Steve Mandanda aliyezaliwa Congo DR, enzi hizo ikiitwa Zaire. Kumbukumbu zinaonesha kuwa Umtiti alizaliwa Novemba 14, 1993 mjini Yaounde, Cameroon na alipofikisha umri wa miaka miwili yeye na familia yake walihamishia makazi yao Ufaransa, katika kitongoji cha Villeurbanne nje kidogo ya mji wa Lyon. Baadae kidogo wakahamia eneo lililopo jirani na hapo lijulikanalo kama Menival ambapo Umtiti alipofikisha umri wa miaka mitano akajiunga na timu ya Menival FC na alipofikisha umri wa miaka minane akajiunga na kituo cha kukuzia vipaji cha klabu ya Lyon.
Kwa mara ya kwanza Agosti 16, 2011 Umtiti alijumuishwa kwenye kikosi cha Lyon walipokuwa wakipambana na Rubin Kazan lakini aliishia benchi hakupata nafasi ya kucheza. Januari 8, 2012, alicheza dakika zote katika ushindi wa 3-1 walioupata mbele ya Lyon-Duchere katika Kombe la Ligi Ufaransa, na mwaka huo ndio ukawa mzuri kwake kwani alifanikiwa kuwepo kwenye kikosi cha kwanza cha Lyon. Kutokana na kiwango bora alichokuwa akikionesha kikawafanya mashabiki wa timu ya Lyon kumchagua kuwa mchezaji bora wa msimu wa mwaka 2012/13 akimpiku Alexandre Lacazette na ilipofikia Juni 30, 2016 akajiunga na Barcelona.
Kwa upande wa Mandanda alizaliwa Machi 28, 1985, katika mji wa Kinshasa na akahamia Evreux, Ufaransa akiwa na umri wa miaka miwili. Awali alijiingiza kwenye mchezo wa ngumi na kuwa bondia mahiri lakini akaamua kuutupilia mbali mchezo huo na kujiunga na timu ya mtaani kwao iliyokuwa ikijulikana kwa jina la ALMEvreux kipindi hiko alikuwa na umri wa miaka minane.
Mlinda mlango huyu ambaye kwa sasa anaidakia klabu ya Marseille aliiwakilisha Ufaransa kwenye michuano ya mataifa ya Ulaya (Euro) mwaka 2008, 2012 na 2016 na mara mbili kwenye Kombe la Dunia mwaka 2010 na 2018. Msimu wa mwaka 2003/06 ndio ulikuwa mwanzo wa mafanikio ya Mandanda katika soka la kulipwa ambapo alianza vizuri msimu kwa kucheza mechi tatu bila kuruhusu bao, kipindi hicho akiidakaia timua ya La Havre.
Alicheza mechi 30 za ligi huku akionekana kuwa bora katika kuhimili mashuti ya washambuliaji, kuokoa michomo hatari na umakini langoni. Mwishoni mwa msimu huo alikwenda England kufanya majaribio kwenye klabu ya Aston Villa lakini hakufanikiwa kufuzu na akajiunga na Marseille katika usajili wa majira ya joto mwaka 2007 na kudumu nayo klabu hiyo mpaka leo.

Comments

Popular posts from this blog

Janga la Yanga si la Kitoto

Mwinyi aongoza maziko ya baba mkwe wa Kikwete

HII NI NEEMA KWA MRISHO MPOTO