Janga la Yanga si la Kitoto

JANGA linaonekana
kuendelea kuwakabili wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya
kimataifa, Yanga yenye maskani yake Jangwani, Dar es Salaam.
Yanga ambao kwa sasa wanaonekana kutokuwa
sawa kiuchumi na kiuongozi pia wamekuwa hawapati matokeo mazuri katika
mechi zao za kimataifa. Mabingwa hao wa msimu wa mwaka 2016/17 walipata
tiketi ya kuiwakilisha nchi mwaka huu kwenye michuano ya kimataifa
wakishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika. Mambo hayakuwa mazuri kwao kwani
walishindwa kuhimili vishindo vya wababe waliokutana nao kwenye michuano
hiyo na kujikuta wakitolewa hatua ya kwanza.
Kutokana na kufika hatua hiyo kanuni ya
Shirikisho la Soka Afrika (Caf) inayosimamia michuano hiyo ikawaruhusu
kuangukia kwenye hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo
huko walipambana hadi wakafanikiwa kuvuka hatua hiyo mpaka kwenye
makundi. Kwenye makundi wamepangwa kundi D pamoja na timu za USM Alger
ya Algeria, Rayon Sports ya Rwanda pamoja na Gor Mahia ya Kenya.
Kwenye hatua hiyo napo hali si hali kwani
kwenye mechi tatu walizocheza mpaka sasa wamejikuta wakiburuza mkia
wakiwa na pointi moja tu huku USM Alger wakiongoza baada ya kupata
pointi saba kwenye michezo yao mitatu, Gor Mahia wenye pointi tano
wanashika nafasi ya pili na ya tatu inakamatwa na Rayon Sports ambao
wenye pointi mbili. Washindi wawili wa kundi ndio watavuka hatua hiyo na
kwenda robo fainali hali inayoonekana kuwa ngumu kwa Yanga kuvuka hapo.
Hesabu ambazo zitawabeba Yanga mpaka hatua
inayofuata ni kuwa wanatakiwa washinde mechi zote tatu ambazo
zitawafanya wafikishe pointi 10 huku wakiombea mmoja kati ya timu
walizonazo kwenye kundi hilo ashinde mechi mbili zilizobakia. Kama USM
Alger watashinda mechi mbili na kupoteza ya Yanga watafikisha pointi 13
ambazo zitawafanya wavuke moja kwa moja.
Rayon ikishinda mechi mbili na kupoteza ya
Yanga itafikisha pointi nane ambazo zitaifanya ivuke na Yanga. Gor
Mahia kama wakishinda mechi mbili na kupoteza ya Yanga watafikisha
pointi 11 ambazo zitawavusha yeye na Yanga. Kuna hesabu tofauti na hizo
ambazo zinaivusha Yanga kwenye hatua hii lakini ni kwenye karatasi tu
zinaonekana kuwa ni rahisi kukupa majibu lakini ni ngumu kwenye dakika
90 kutokana na kila timu kujipanga kivyake kuhakikisha kwenye raundi hii
ya lala salama hawapotezi mchezo wowote kirahisi.
Mpaka sasa Yanga wameshacheza mechi tisa,
kwenye michezo yote hiyo wamevuna pointi tisa tu, wameshinda mbili,
wamefungwa nne na sare tatu. Safari ya Yanga ilikuwa hivi kimataifa
Februari 10, 2018 Tarehe hiyo walikuwa na kibarua cha hatua ya awali ya
Ligi ya Mabingwa Afrika, wakashuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, kucheza na Saint Louis na wakaibuka na ushindi wa bao 1-0
lililofungwa na Juma Mahadhi dakika ya 67 na waliporudiana kwenye Uwanja
wa Linite, Victoria visiwani Shelisheli walitoka sare ya kufungana bao
1-1.
Machi 6, 2018 Baada ya matokeo hayo
wakavuka mpaka hatua ya kwanza ambapo walikutana na Township Rollers
wababe kutoka Botswana. Hapa wakakwaa kisiki baada ya mchezo wa kwanza
hapa Dar es Salaam kukubali kipigo cha mabao 2-1 Machi 17, 2018 Tarehe
hiyo timu hizi zilicheza mechi yao ya marudiano mjini Gaborone, wakatoka
suluhu na kuwafanya watolewe kwenye michuano hiyo na kuangukia Kombe la
Shirikisho. Aprili 7, 2018 Baada ya kuangukia kwenye Kombe la
Shirikisho wakapangiwa kukutana na Welayta Dicha kutoka Djibout.
Kwenye mchezo wa kwanza walijitutumua na
kuibuka na ushindi wa 2-0. Aprili 18, 2018 Wakarudiana na Dicha na hapa
Yanga wakafungwa 1-0 lakini matokeo haya hayakuwanyima nafasi ya kutinga
hatua ya makundi. Mei6, 2018 Walicheza mchezo wao wa kwanza na USM
Alger mjini Algiers kwenye Uwanja wa 5 Juilete 1862 na kukubali kipigo
cha mabao 4-0. Mei 16, 2018 Wakiwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
wakashindwa kupata pointi tatu mbele ya Rayon Sports baada ya kumaliza
dakika 90 suluhu. Julai 18, 2018 Wakiwa Uwanja wa Moi, Nairobi, Kenya
wakakumbwa na kipigo kingine cha mabao 4-0 ukiwa ni muendelezo wa
matokeo mabaya kwa klabu hiyo.
Kazi ngumu inausubiri Yanga mbele ili kusonga mbele, ama imalize hatua ya makundi na kujipanga na msimu mwingine wa ligi.
Comments
Post a Comment