Mashtaka watakiwa kutekeleza maagizo ‘Mpemba wa Magufuli

Picha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa siku sita kwa upande wa mashitaka katika kesi ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo inayomkabili mfanyabiashara Yusuf Ali “Mpemba wa Magufuli” kutoa taarifa ya utekelezaji wa maagizo, likiwemo la Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alitoa amri hiyo jana baada ya Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde kudai kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi umekamilika.
Pia alidai kuwa wapo katika utekelezaji wa maelekezo waliyopewa na DPP. Wakili wa Utetezi, Nehemia Nkoko alidai kuwa ahadi za upande wa mashitaka katika kesi hiyo ni za kawaida, hivyo wanaomba kujua washitakiwa hao watasomewa lini maelezo ya mashahidi.
Hata hivyo, Hakimu Simba alisema mpaka wiki ijayo wawe wameeleza kesi hiyo imefi kia wapi na kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 24, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Julai 5, mwaka huu, upande wa mashitaka uliieleza mahakama kuwa wanalifanyia kazi jalada la kesi hiyo baada ya kupewa maelekezo na DPP.
Mbali na Yusuph, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Charles Mrutu, mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima wa Mbezi, Ahmed Nyagongo, dereva na Pius Kulagwa. Washitakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka manne ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6 na upelelezi wa kesi hiyo umekwishakamilika.
Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016 wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola za Marekani 180,000 (Sh milioni 392.8) bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Comments

Popular posts from this blog

Janga la Yanga si la Kitoto

Mwinyi aongoza maziko ya baba mkwe wa Kikwete

HII NI NEEMA KWA MRISHO MPOTO