Marekani yaguswa na ujio wa Dreamliner

Picha
UBALOZI wa Marekani nchini umesema unaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika ununuzi wa ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner katika kukuza uchumi wa taifa.
Katika kuonesha kwa vitendo kuunga mkono juhudi hizo za serikali ya Rais John Magufuli, imesema kwamba Julai 29, mwaka huu, itatumia ndege hiyo katika safari yake ya kwanza kwenda Arusha na Mwanza. Aidha, ubalozi huo umeshauri Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kuwekeza kwenye kuendeleza wataalamu watakaohudumia ndege hiyo kwa kuwa imeundwa kwa teknolojia kubwa na ya kisasa.
Hayo yalibainishwa jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk Inmi Patterson wakati alipotembelea ndege hiyo ambayo inatarajiwa kuanza safari zake za ndani mwishoni mwa mwezi huu.
Dk Patterson alisema ndege hiyo ni kubwa na ina vitu vinavyovutia ndani na ili kuona uzuri zaidi wa ndege hiyo, itakapoanza safari yake ya kwanza atasafiri kwa ndege hiyo, ikiwa ni njia ya kuunga mkono serikali na ATCL.
“Ndege ni kubwa, nzuri na ya kuvutia nataka kupata uzoefu zaidi kwa safari yake ya kwanza nataka kuona kila kitu kwenye Dreamliner,” alisema Dk Patterson.
Akifafanua ATCL kuendeleza wataalamu watakaohudumia, alisema ndege hiyo imeundwa kwa teknolojia kubwa hivyo ni muhimu kwa shirika hilo kuendeleza wataalamu watakaohudumia ndege hiyo, lengo likiwa ni wao kuendana na teknolojia iliyotumika.
“Biashara ya ndege ina changamoto na ili kuendana nayo ni muhimu kuwekeza kwa wataalamu, teknolojia iliyopo huku ni kubwa na sio rahisi wote watakaofanya kazi huku ni lazima waendelezwe ili kuendana na teknolojia iliyopo,” aliongeza.
Ndege hiyo iliyonunuliwa na serikali yenye uwezo wa kubeba abiria 262, iliwasili nchini Julai 8, mwaka huu na inatarajiwa kuanza safari zake Julai 29, kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro na Mwanza.
Aidha, imeelezwa kuwa kuanzia Septemba mwaka huu, ndege hiyo itaanza safari zake kwenda Bombay- India, Guangzhou-China na Bangkok -Thailand, na kwamba utaratibu umeanza ili ndege hiyo ifanye safari kwenda Uingereza na miji mingine duniani.
Hii ni ndege ya nne kununuliwa na serikali ikitanguliwa na Bombardier Q-Dash 8 na huku nyingine mbili zikitarajiwa kuingia nchini kabla ya mwaka huu kumalizika, na ndege nyingine kubwa ya pili ya 787-7 Dreamliner ikitarajiwa kuwasili nchini 2020.

Comments

Popular posts from this blog

Janga la Yanga si la Kitoto

Mwinyi aongoza maziko ya baba mkwe wa Kikwete

HII NI NEEMA KWA MRISHO MPOTO